Watu wengi wanafikiri mtu kuwa mjasiliamali ni
lazima uende shule kusoma madigrii mengimengi, uwe na mtaji wa mapesa
mengimengi, hapana, ujasiliamali ni kuchukua hatua ya kutumia fursa
zinazokuzunguka.
Katika makala haya nakuletea tabia 10 ambazo ni
dalili tosha kwamba wewe ni mjasiriamali na kama huna tabia hizi usisononeke
maana unaweza ukaanza kujifunza taratibu na baadae ukawa na tabia za
kijasiriamali.
Kama unatabia hizi 10, ni dalili tosha
kwamba wewe una damu ya mjasiriamali, unatakiwa kuchukua hatua mara moja ili
kufikia mafanikio makubwa;
1. Hukubaliani na mfumo. Mara nyingi umekuwa
ukihoji kwa nini kitu fulani kifanyike na umekuwa ukijitahidi kutafuta njia
bora zaidi ya kufanya kazi fulani pale unapokuwa umeajiriwa. Hufanyi kitu bila
ya kuhoji umuhimu wake na kufikiri njia ya kuboresha.
2. Unaonekana kama mfanyakazi mkorofi. Wakati
mwingine umeshafukuzwa kazi mara kadhaa kutokana na tabia yako ya kuhoji na
kutaka kuboresha utendaji kazi. Au umeshaacha kazi au kupanga kufanya hivyo
kutokana na kutoridhishwa na kazi hiyo.
3. Una hamasa kubwa ya kutekeleza majukumu yako.
Husubiri upangiwe cha kufanya, unajua majukumu yako na unayafanya kwa ubora wa
hali ya juu.
4. Ukiambiwa hapana huridhiki, hapana sio jibu
kwako unaendelea kutafuta njia nyingine mpaka upate NDIYO.
5. Unajiamini na unaamini una uwezo mkubwa wa
kufanya mambo makubwa. Una uhakika hata kitokee kitu gani bado unauwezo wa
kusimama na kuleta tofauti.
6. Ni mtu wa watu, unaweza kuchangamana na watu
wa aina zote. Huna ubaguzi wa aina gani ya watu unaweza kukaa nao, popote
unapokutana na watu unaweza kuanzisha mazungumzo na mkaenda vizuri.
7. Huogopi sana juu ya usalama wa ajira kwani
unaamini hata bila ya ajira bado unaweza kuendesha maisha yako.
8. Mara kadhaa umekuwa ukigomea mamlaka. Umekuwa
ukikataa maelekezo yanayotolewa na mamlaka kama hayaendani na misimamo yako ya
ufanyaji kazi bora. Hii imekupelekea kuonekana ni mfanyakazi mkorofi na hata
kufukuzwa.
9. Siku za mapumziko kama sikukuu au mwisho wa
wiki ndio siku bora kwako kufanya kazi zako binafsi, huendekezi kupoteza muda
kwa kupumzika au kustarehe.
10. Umewahi kuuza vitu vidogo vidogo ulipokuwa
mtoto. Pia umewahi kufuga kuku, sungura na hata njiwa enzi za utoto wako.

No comments:
Post a Comment